Rais wa Ufaransa ametangaza kuwa wanajeshi wa nchi hiyo watarejeshwa nyumbani kutoka Niger baada ya serikali mpya ya Niamey kukata uhusiano wake wa kijeshi na mkoloni huyo kizee wa barani Ulaya.
Kwa mujibu wa televisheni ya Al Jazeera, Emmanuel Macron alisema hayo jana jioni na kudai kuwa wameamua kumuondoa balozi wao nchini Niger na kusitisha uhusiano wao wa kijeshi na nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Matamshi hayo ya rais wa Ufaransa yamekuja kwa kuchelewa sana baada ya balozi wa Ufaransa na wanajeshi wa nchi hiyo kutimuliwa huko Niger.
Macron anadai kuwa wao ndio walioamua kumrejesha nyumbani balozi na wanajeshi wao kutoka Niger katika hali ambayo muda wote huu Paris ilikuwa inafanya ukaidi wa kuondoka katika nchi hiyo ya Afrika licha ya kufukuzwa, kukatiwa maji, umeme na chakula na licha ya kupigwa marufuku mtu yeyote kushirikiana na ubalozi wa Ufaransa mjini Niamey.
Mataifa ya rais wa Ufaransa yamekuja baada ya kufanyika maandamano makubwa ya mara kadhaa ya wananchi wa Niger ya kutaka wanajeshi wa mkoloni huyo wa Ulaya na balozi wake waondoke kwenye ardhi ya Niger.
Kwa mujibu wa Macron, wanajeshi 1,500 wa Ufaransa wataondoka nchini Niger katika kipindi cha wiki na miezi ijayo na watakuwa wote wameshaondoka nchini humo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2023.