Israel siku ya Ijumaa ilitetea ulazima wa kijeshi wa mashambulizi yake Gaza katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki baada ya Afrika Kusini kuwataka majaji kuiamuru kusitisha operesheni huko Rafah na kujiondoa kabisa katika ardhi ya Palestina.
Afisa wa Wizara ya Sheria ya Israel Gilad Noam aliitaja kesi ya Afrika Kusini, ambayo inaishutumu Israel kwa kukiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari, “iliachana kabisa na ukweli na mazingira.”
“(Kesi) inafanya mzaha kwa shtaka la kutisha la mauaji ya halaiki,” Noam alisema.
Kabla ya wasilisho la Israel, waandamanaji kadhaa wanaoiunga mkono Israel walikusanyika nje, wakionyesha picha za mateka zilizopigwa na wapiganaji wa Hamas mnamo Oktoba 7 na kutaka waachiliwe.
Siku ya Alhamisi, balozi wa Afrika Kusini nchini Uholanzi, Vusimuzi Madonsela, aliiomba mahakama iamuru Israel “kuondoa mara moja, kikamilifu na bila masharti, jeshi la Israel kutoka eneo lote la Ukanda wa Gaza.”