Rais wa Nigeria Bola Tinubu ameviagiza vikosi vya usalama kutolipa fidia kwa ajili ya kuwaachilia wanafunzi wapatao 300 na wafanyakazi waliotekwa nyara kutoka shuleni kaskazini-magharibi mwa jimbo la Kaduna wiki iliyopita.
Bw Tinubu badala yake aliagiza mashirika ya usalama kuhakikisha kuwa waathiriwa wote waliotekwa nyara wameachiliwa bila malipo yoyote kwa watekaji nyara, Waziri wa Habari wa nchi hiyo Mohammed Idris aliambia wanahabari Jumatano.
Bw Idris alisema rais aliwaambia vikosi vinavyowatafuta wanafunzi kuhakikisha “hakuna hata senti moja inayolipwa”.
Hapo awali, watu wenye silaha walikuwa wamewateka nyara wanafunzi 286 na wafanyakazi kutoka shule moja kaskazini mwa Nigeria wiki iliyopita wamedai jumla ya naira bilioni 1 ($620,432) ili waachiliwe, msemaji wa familia za mateka na diwani wa eneo hilo waliambia Reuters.
Watoto hao wa shule, baadhi ya wanafunzi wakubwa na wafanyakazi wa shule hiyo walitekwa nyara mnamo Machi 7 katika mji wa Kuriga, kaskazini magharibi mwa Jimbo la Kaduna nchini Nigeria, katika tukio la kwanza la utekaji nyara nchini humo tangu 2021.