Misri leo imefungua mkutano wa kilele wa amani kuhusu mzozo wa Gaza kama sehemu ya majaribio ya kumaliza vita vya kikanda.
Viongozi wa Mashariki ya Kati na Ulaya wanakusanyika mjini Cairo kwa ajili ya mkutano huo, lakini kuna uwezekano wa kutatiza kuafikiana juu ya mzozo kati ya Israel na Hamas.
Wakati wa hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo, Rais wa Palestina Mahmoud Abbas alisema “hatutaondoka, tutabaki kwenye ardhi yetu”.
Zaidi ya watu milioni moja wa Gaza waliambiwa waondoke makwao katika Jiji la Gaza na maeneo jirani huku Israel ikipanga kufanya mashambulizi ya ardhini.
Wakati huo huo, Rais wa Misri Abdel Fattah al Sisi amesema amewaalika viongozi kufikia makubaliano ya kupata ramani ya njia ya kumaliza maafa ya kibinadamu huko Gaza na kufanya mazungumzo ya amani.
Wanadiplomasia wawili waliliambia shirika la habari la Reuters kuwa hakuna uwezekano kuwa kutakuwa na taarifa ya pamoja kutoka kwa mkutano huo kwa sababu ya hisia kuhusu wito wowote wa kusitisha mapigano.
Kutokuwepo kwa Marekani na viongozi wengine wakuu wa nchi za Magharibi pia kumepunguza matarajio ya kile ambacho tukio hilo linaweza kufikia.