Kundi la wanamgambo wa Lebanon Hezbollah limeapa kulipiza kisasi kwa mashambulizi hayo yaliyotokea katika mji wa Nabatiyeh na kijiji kimoja kusini mwa Lebanon saa chache baada ya makombora kutoka Lebanon kumuua mwanajeshi wa Israel.
Akitoa taarifa hiyo afisa mkuu wa Hezbollah na mbunge Hassan Fadlallah alisema siku ya Alhamisi kwamba Israel itakabiliwa na kisasi baada ya mashambulio mawili yaliyofanyika kusini mwa Lebanon siku iliyotangulia kuwaua raia 10, nusu yao ikiwa ni watoto.
“Adui (Israel) italipa gharama ya uhalifu huu,” Fadlallah aliiambia Reuters alipoulizwa kuhusu majibu ya kundi hilo lenye silaha.
Idadi ya vifo vya raia kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel nchini Lebanon imeongezeka na kufikia angalau 10, vyombo vya habari vya serikali ya Lebanon viliripoti Alhamisi, na kuifanya siku iliyotangulia kuwa mbaya zaidi katika kipindi cha zaidi ya miezi minne ya mapigano ya kuvuka mpaka.