Hezbollah ilirusha msururu wa makombora kuelekea kaskazini mwa Israel Jumapili usiku, huku wanajeshi wa Israel wakiwa katika hali ya tahadhari ya kulipizwa kisasi kutoka kwa Iran na washirika wake kufuatia mauaji ya kiongozi mkuu wa Hamas mwezi uliopita.
Milio ya roketi kuelekea Israel na wanamgambo wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran kusini mwa Lebanon imekuwa tukio la karibu kila siku tangu kuzuka kwa vita huko Gaza, huku hofu ikiongezeka juu ya uwezekano wa shambulio la Irani ambalo linaweza kuongezeka na kuwa mzozo mkubwa zaidi wa kikanda.
Haya yanajiri baada ya Shirika la Habari la Taifa la Lebanon kuripoti kwamba shambulizi la Israel katika mji wa Ma’aroub, kusini mwa Lebanon, lilijeruhi watu 12 wakiwemo watoto sita.
Takriban roketi 30 zilirushwa kutoka Lebanon, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema, na kuongeza kuwa baadhi zilianguka katika maeneo ya wazi na hakuna majeraha yaliyoripotiwa.
Mapema Jumapili, IDF ilisema maagizo yake kwa umma hayajabadilika huku kukiwa na uwezekano wa majibu ya kijeshi kutoka kwa vikosi vya Iran kwa mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh huko Tehran mnamo Julai 31.