Wakili wa utetezi katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa Rais wa (TFF) Jamal Malinzi na wenzake ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuamuru upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi wa kesi hiyo.
Hayo yameelezwa na wakili wa utetezi, Nehemiah Nkoko mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Leonard Swai kueleza upelelezi haujakamilika.
Swai amedai kuwa kesi ya Malinzi na wenzake imeitishwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika, hivyo anaomba iahirishwe. Kutokana na hatua hiyo, Wakili Nkoko amedai kuwa kesi hiyo imechukua muda mrefu na kila siku wanaambiwa jalada bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Ameeleza kuwa ni miezi miwili imepita sasa anaiomba mahakama itumie uwezo wake kuiharakisha kesi hiyo ili iweze kuanza kusikilizwa na kuendelea kuwa upande wa mashtaka umewafungulia washtakiwa kesi ya utakatishaji ili kuwakomoa hivyo wanatumia kesi hiyo kama ngao ya ukandamizaji.
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Mashauri amesema mahakama hiyo inafanya kazi ya kutafsiri sheria na kama itafanya vinginevyo itakuwa nje ya sheria. Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi January 11, 2018.
MAHAKAMANI: Kesi ya Aveva na Malinzi