Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli, Askofu Frederck Shoo amewata baadhi ya watu kuacha kupotosha ukweli wa waraka wa maaskofu kwa kuupaka matope na kusema anae fanya hivyo ni mjinga.
Askofu Shoo ametoa kauli hiyo leo April 1, 2018 katika Usharika wa Moshi Mjini Dayosisi ya kaskazini, mkoani Kilimanjaro wakati akitoa salamu za Pasaka.
Askofu Shoo amenukuliwa akisema “Wapo wanaotumia nguvu nyingi kutaka kupotosha ujumbe wa waraka wa Maaskofu na wamekuwa wakilipaka Kanisa matope ili waweze kurejea katika waraka ule, watu hawa naweza kuwaita ni wajinga lakini pamoja na hilo nataka wakayatafakari na kama wanaona kuna hatua za kuchukua wachukue.”
“Kanisa limekuwa linapata kejeli za aina mbalimbali kutoka kwa watu hao na kuwatuhumu kuwa maskofu walifikia maamuzi ya kuandika waraka huo kutokana na sababu za kimaslahi kwa maana ya sadaka makanisani kupungua jambo ambalo si la kweli.” -Askofu Shoo
“Kanisa linasitikika sana, tunaposema jambo la kweli na jambo linalohusu maisha ya Watanzania wote, halafu kunatokea watu chache ambao naweza kuwaita wajinga wanakebehi na kusema eti kwa sababu sadaka zimepungua kanisani sisi sadaka hazijapungua kwani wakristo wanajitoa sana na hatujapungukiwa na kitu ila tunasema yale tunayoyaamini,” -Askofu Shoo
“Najua tutaitwa majina mengi maaskofu na hizo ni jitihada za upotoshaji wa ule ukweli ulipo katika waraka na tukumbuke hili si jambo la hivi hivi tu.. kwani kwa wakati mmoja mabaraza ya maaskofu wa makanisa makubwa mawili nchini kukaa na kutoa waraka ambao una ujumbe ulioshabihiana si kitu cha kawaida mimi nasema kuna kitu Mungu anataka kutuambia kupitia ujumbe ule tutafakari hili kama taifa,” -Askofu Shoo