Leo March 16, 2018 Watu watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya kuwaingiza nchini kimagendo wahamiaji haramu na kughushi vyeti vya kuzaliwa.
Watu hao ni Mfanyabiashara Abdulkadir Salah (37) ni dereva, Said Mtambo (34) ni kondakta, Hassan Mgeni ( 41) na madalali Issa Juma na Mohammed Ngotyagayi.
Wakisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, Mwendesha Mashtaka wa Uhamiaji, Novatus Mlay amedai kuwa washtakiwa wametenda kosa hilo March Mosi, 2018 Makao Mkuu ya Uhamiaji Temeke.
Inadaiwa mshtakiwa Abdulkadir Salah aliwaingiza nchini kimagendo Aden Ibrahim, Liban Gulet na Mohammed Ibrahim ambao ni raia wa Somaria.
Mlay amedai kuwa siku hiyo ya March Mosi,2018 mshtakiwa Salah alikamatwa akiwa nchini bila ya kuwa na hati ya kusafiria pamoja na Visa.
Mbali na mashtaka hayo mshtakiwa Salah anadaiwa kukutwa na nyaraka zilizoghushiwa ambazo ni vyeti vya kuzaliwa namba BB/NO 0094366 chenye jina la Ahmed Mursal, BB/NO 0418995 Hadija Athuman na BB/NO0419004 Ally Abdi kwa lengo la kupata hati za kusafaria.
Kwa upande wa washtakiwa Said, Hassan, Issa na Mohammed wao wanakabiliwa na shtaka la kusaidia kuwaingiza nchini kimagendo wahamiaji haramu ambao ni raia wa Somalia.
Inadaiwa washtakiwa hao walisaidia kuwaingiza kimagendo nchini Aden Ibrahim, Libyan Gullet na Mohammed Ibrahim.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa wote wamekana na upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Hakimu Shaidi ametoa masharti ya dhamana ambapo amemtaka mshtakiwa Abdulkadir kuwasilisha hati yake ya kusafiria mahakamani ama kuwa na mdhamini ambaye ni raia wa Tanzania ambaye atawasilisha mahakamani hati ya mali isiyohanishika.
Kwa upande wa washtakiwa wengine wawe na wadhamini wawili wenye barua na vitambulisho ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh.Milioni 5.
Mshtakiwa Said na Hassan wamekamilisha masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi March 28,2018.
‘NABII ANAEGAWA HELA SHILLAH’ AZUNGUMZA KANISA KUFUTIWA USAJILI, KUITWA DODOMA