Watu Sita akiwemo mtoto wa aliyekuwa Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova (Masoud Kova) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wa kuisababishia hasara ya Shilingi Milioni 26 Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
Mbali ya Kova ambaye ni Account Technician wa TPA, washtakiwa wengine ni Lydia Kimaro (52), Ally Mkango (54) ni Operate Officer wa TPA na Aron Luisinga (35) Account Technician TPA.
Pia Grace Komba (41) na Juma Ng’oka (41) ambao ni Maofisa wa Benki ya CRDB.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao na wakili wa serikali, Mwanaamina Kombakono mbele ya Hakimu Mkazi Mkuuu, Thomas Simba ambapo amedai washtakiwa wanakabiliwa na makosa matano.
Wakili Kombakono amedai kuwa kosa la kwanza ni kughushi ambapo linamkabili mshtakiwa Kimaro na Kova, ambapo wanadaiwa kati ya August na September 2014 katika mkoa wa DSM wakiwa na nia ya kudanganya walighushi nyaraka za uongo ili kuonyesha TPA imehusika katika malipo ya kiasi cha Sh.Mil 26 kutoka kwa Cargo Service Invoice (CSI) hali ya kuwa si kweli.
Katika shtaka la pili ambalo ni kughushi, linamkabili Kimaro na Kova wakidaiwa kati ya August na September 2014 katika mkoa wa DSM, wakiwa na nia ya kudanganya walighushi nyaraka kuonyesha TPA imehusika na malipo ya Sh.Mil 26 kutoka Kampuni ya Freight Forwarders (T) hali ya kuwa ni uongo.
Wakili Kombakono amedai kuwa shtaka la tatu ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ambalo linawakabili washtakiwa wote, ambapo wamelitenda kosa hilo kati ya September na October 2014 maeneo ya Dar es Salaam.
Inadaiwa kwa pamoja walijipatia kiasi cha Sh.Mil 26 kutoka kwa Freight Forwarders na kudanganya kuwa pesa hiyo imelipwa katika akaunti ya TPA iliyopo benki ya CRDB hali ya kuwa ni uongo.
Kosa la nne ni kushindwa kuzuia kosa, ambapo linamkabili mshtakiwa Mkango na Lusingu ambapo wanadaiwa wametenda kosa hilo kati ya September na October 2014 maeneo ya Dar es Salaam.
Inadaiwa wakiwa waajiriwa wa TPA walishindwana kuzuia kutendeka kwa kosa kwa kutokagua upande wa TPA na Cargo Service Invoice (CSI) hali iliyosababisha Freight Forwarders kutoa makontena 16 bila kulipiwa kodi ya Sh.mil 26 kwa TPA.
Kosa jingine ni kuisababisha hasara mamlaka, ambapo linawahusu washtakiwa wote, wakidaiwa kati ya September na October 2014 maeneo ya Dar es Salaam kwa pamoja na kwa nia ovu wameisabibishia TPA kuingia hasara ya Sh.Mil 26.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hao wamekana makosa yao ambapo Wakili Kombakono amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Wakili wa utetezi Emmanuel Muga, aliiomba mahakama iwapatie wateja wake dhamana, ambapo Hakimu Simba ametoa masharti ya washtakiwa kuwa na wadhamini 2, watakaotoa fedha taslimu Sh. Mil 2 na laki 2/ mali isiyohamishika, pia wawasilishe hati zao za kusafiria mahakamani na wasitoke nje ya jiji la DSM bila kibali cha mahakama.
Washtakiwa walitimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana, ambapo Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi April 25,2018 kwa ajili ya kutajwa.
BREAKING; Mabehewa Manne ya Treni yamepata ajali Katavi (VIDEO)