Karibu kuitazama historia fupi ya Daniel Arap Moi ambaye alitawala siasa za Kenya kwa zaidi ya robo karne.
Yeye alikuwa mwanasiasa aliyetaka kupendwa zaidi na wananchi kuliko alivyokuwa mtangulizi wake, rais wa kwanza wa jamuhuri ya Kenya Mzee Jomo Kenyatta.
Hata hivyo alishindwa kuvunjilia mbali utawala wa kiimla wa Jomo Kenyatta na badala yake yeye mwenyewe akajikuta katika hali ya kuwadhulumu wapinzani wake wa kisiasa.
Alibatizwa jina la “Profesa wa Siasa” kwa vile alivyoweza kukabiliana na wapinzani wake. Hata hivyo utawala wake ulimalizika na sifa mbaya kwa kuwa Serikali yake ilidumaza uchumi na ufisadi ukashamiri.
Moi alizaliwa Septemba 2, mwaka 1924, katika jamii ya wakulima katika kaunti ya Baringo, katikati magharibi mwa Kenya.
Jina lake la kwanza lilikuwa Toroiticha arap (mwana wa) Moi lakini baadaye akabatizwa katika Ukristo na kupewa jina la Daniel. Alipewa jina hilo la Wamishenari Wakristo akiwa mwanafunzi.