Hospitali mjini Khartoum nchini Sudan zimeelemewa na majeruhi kutokana na mapigano kati ya jeshi la Sudan na Rapid Suport Forces (RSF) yaliyoanza wiki iliyopita na kusababisha vifo vya mamia ya watu huku maelfu wakiukimbia mji huo.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya hospitali kufungwa na wagonjwa kuhamishwa katika hospitali nyingine hali kadhalika madaktari nao wanatoka hospitali moja hadi nyingine. Daktari huyo amesema “hali ni mbaya sana, sijalala siku ya pili leo, majeruhi ni wengi na tuna uhaba wa wafanyakazi na kusema kuwa wamekuwa wakipokea msaada wa vifaa kutoka wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF)”Dk. Omar
Mapigano makali katika mji huo Khartoum yalisababisha ugumu kwa watu kufikia huduma za msingi wakati hospitali zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa wafanyakazi, madaktari, umeme, mafuta na “kila kitu kasoro waathirika” alisema.
Licha ya mapigano ya hapa na pale, Marekani imeweza kusimamia sitisho la mapigano la saa 72 kati ya majenerali wawili waliohasimiana, huku wakazi wa mji huo wanatumia hali ya utulivu uliopo kukusanya tena mahitaji muhimu au kuondoka mjini Khartoum.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken Jumatatu alitangaza kwamba pande zinazo zozana nchini Sudan zimekubaliana kusitisha mapigano kwa saa 72.
Alisema Marekani itashirikiana na washirika wa kikanda na wa kimataifa na wadau wa kiraia wa Sudan kusaidia kuunda kamati yenye lengo la kupatikana kwa “sitisho la kudumu la mapigano na kuweka mipango ya masuala ya kibinadamu nchini Sudan.”
Katika taarifa ya maandishi ya Jumatatu, RSF ilisema imekubali kusitisha mapigano “ili kufungua njia za kibinadamu, kuwawezesha raia na wakaazi kutoka na kwenda kujipatia mahitaji yao muhimu, kwenda hospitali na maeneo salama na kuwezesha balozi kuwaondoa wafanyakazi wao.”