Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuhukumu kifungo cha nje cha mwaka mmoja, Mkurugenzi wa Jamii Forums Maxence Melo baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuzuia Askari Polisi kutekeleza majukumu yake.
Mahakama hiyo pia imemuachia huru mshtakiwa Mike Mushi kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake, huku ikimuonya Melo kutofanya kosa lolote ndani ya mwaka mmoja.
Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi huku upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Faraji Ngukah.
Katika hukumu hiyo, Hakimu Shaidi amesema mahakama inamuhukumu Melo kifungo cha nje cha mwaka mmoja baada ya kutiwa hatia kwa kosa la kuzuia Jeshi la Polisi kutekeleza majukumu, pia inamuachia huru Mushi ambaye alionekana kama msindikizaji katika kesi hiyo.
Hukumu hiyo imetolewa baada ya Upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao kwa kuleta mashahidi sita huku Melo akijitetea mwenyewe bila kuwa na shahidi mwingine.
Awali kabla ya kusomwa hukumu hiyo Wakili Faraja Ngukah aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa kwani kitendo alichokifanya cha kuzuia askari kutekeleza majukumu yao ni hatari kwa Taifa.
Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Bernedict Ishabakaki aliiomba mahakama itoe hukumu ya faini kwa sababu washitakiwa ni vijana ambao wameajiri na wanategemewa hivyo faini itakuwa fundisho.
Baada ya kusikiliza hoja hizo Hakimu Shaidi alisema mshtakiwa alionekana kuwa na makosa katika kesi ambazo zilifunguliwa awali ambazo zote zilikuwa na makosa yanayofanana.
“Jeshi la Polisi liko kwa ajili yetu sote kazi yaje ni kupelelza na sisi ni wajibu wetu kushirikkiana nalo na mahkaama inaweza kukumbusha hilo,” Hakimu Shaidi na baadaye akasoma hukumu hiyo.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Melo na Mushi walidaiwa kuendesha mtandao ambao haujasajiwa kwa kikoa (domain) cha .tz na katika shtaka jingine walidaiwa kuzuia askari Polisi kutekeleza majukumu yao, makosa wanayodaiwa kuyatenda kati ya Desemba 9, 2011 na Desemba 13, 2016 katika eneo la Mikocheni, wilaya ya Kinondoni.