Rais wa Ukraine amesema “haitafaa” kufanya uchaguzi wakati nchi hiyo ikisalia vitani.
Sheria ya kijeshi ilitangazwa nchini Ukraine wakati uvamizi wa Urusi ulipoanza Februari 2022, ikikataza kufanyika kwa uchaguzi, lakini kumekuwa na mjadala ndani na nje ya nchi kuhusu uwezekano wa kura ya maoni mwezi Machi 2024.
Seneta wa chama cha Republican nchini Marekani Lindsey Graham na maafisa wengine wa nchi za Magharibi walikuwa wameitaka Kyiv kupiga kura kuonyesha kuwa inaweza kufanya uchaguzi huru na wa haki wakati wa vita.
Mwishoni mwa juma, waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba alisema rais anatathmini faida na hasara za uchaguzi wa wakati wa vita.
Lakini katika hotuba ya video ya jana usiku, Volodymyr Zelenskyy alisema: “Sote tunaelewa kuwa sasa, wakati wa vita, wakati kuna changamoto nyingi, ni kutowajibika kabisa kujihusisha na mada zinazohusiana na uchaguzi kwa njia ya kipuuzi.
“Tunahitaji kutambua kwamba huu ni wakati wa ulinzi, wakati wa vita, ambao hatima ya serikali na watu wake inategemea… Ninaamini kuwa uchaguzi haufai kwa wakati huu.”