Mahakama ya kimataifa ya makosa ya uhalifu, ICC inataraji hii leo kutoa maamuzi kuhusu ombi la dharura la Ukraine la kutaka Urusi isitishe mara moja uvamizi wake, huku serikali ya mjini Kyiv ikidai kuwa Urusi ilimtuhumu kwa uongo jirani yake huyo anayeunga mkono nchi za Magharibi kwa mauaji ya halaiki ili kuhalalisha vita hivyo.
Hata hivyo Urusi kwa upande wake ilidai kuhalalisha matumizi ya nguvu dhidi ya Ukraine kwa lengo la kujilinda.
Hukumu hiyo itatolewa mjini The Hague baada ya Ukraine kuwasilisha ombi hilo la dharura muda mfupi baada ya shambulizi la Urusi la Februari 24.
Kyiv inaitaka mahakama hiyo kuchukua hatua za muda mfupi kwa kuiagiza Urusi kusimamisha operesheni zake mara moja wakati idadi ya wakimbizi kutoka Ukraine wakipindukia milioni 3 huku majeshi ya Urusi yakizidisha mashambulizi kwenye majengo ya makazi mjini Kyiv.