Shirika la Afya Duniani liimetangaza kuwa, idadi ya visa vilivyorekodiwa vya maambukizo ya kipindupindu kote ulimwenguni vimeongezeka mara mbili katika mwaka uliopita.
Milipuko ya kipindupindu inaripotiwa zaidi katika nchi za Afghanistan, Cameroon na Congo.
Shirika la Afya Duniani limetangaza katika taarifa yake mjini Geneva kwamba, idadi ya wagonjwa wa kipindupindu imeongezeka zaidi ya mara mbili katika mwaka uliopita. Mnamo mwaka 2022, kesi 470,000 za kipindupindu zilirekodiwa ulimwenguni kote, wakati mnamo 2021, idadi hii ilikuwa 220,000.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, kama ilivyo kawaida, takwimu hizi sio halisi na idadi ya kesi zilizoambukizwa ni kubwa zaidi kuliko takwimu hizi.
Shirika la Afya Duniani linakadiria kuwa kuna visa kati ya 1,300,000 na 4,000,000 vya kipindupindu duniani kila mwaka, na takriban watu 143,000 hufa kutokana na ugonjwa huo kila mwaka.
Kadhalika ugonjwa wa kipiindupindu umo katika hali ya kusambaa barani Afrika; Wizara ya Afya ya Sudan ilitangaza kuandikishwa kwa vifo 18 kutokana na ugonjwa wa kipindupindu katika jimbo la Al-Qadarif mashariki mwa nchi hiyo na visa 265 vinavyoshukiwa kuwa ni vya ugonjwa huo.
Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika limesema katika ripoti yake ya mwezi Agosti kwamba, ugonjwa wa kipindupindu umeziathiri nchi 15. Hivi karibuni kumeripotiwa kuibuka ugonjwa wa kipindupindu katika baadhi ya nchi za Afrika.