Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega leo amewasilisha Bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka 2023/ 2024 ambapo amesema katika mwaka 2022/2023, idadi ya mifugo nchini imeongezeka kutoka ng’ombe milioni 35.3 hadi ng’ombe milioni 36.6, mbuzi kutoka milioni 25.6 hadi milioni 26.6 na kondoo kutoka milioni 8.5 hadi milioni 9.1.
“Kuku pia wameongezeka kutoka milioni 92.8 hadi milioni 97.9 ambapo kuku wa asili wameongezeka kutoka milioni 42.7 hadi milioni 45.1, kuku wa kisasa kutoka milioni 50.1 hadi milioni 52.8 na nguruwe kutoka milioni 3.4 hadi milioni 3.7, aidha ukuaj wa Sekta ya Mifugo kwa mwaka 2021 umefikia asilimia 5.0 na kuchangia asilimia 7.0 kwenye Pato la Taifa”
“Katika mwaka 2022/2023 ng’ombe 2,218,293 na mbuzi/kondoo 2,121,187 wenye thamani ya Shilingi trilioni 1.7 waliuzwa katika minada mbalimbali hapa nchini ikilinganishwa na ng’ombe 2,194,937; mbuzi/kondoo 1,782,010 wenye thamani ya Shilingi trilioni 1.5 waliouzwa katika mwaka 2021/2022”
Kwa upande mwingine amesema uzalishaji wa nyama umeongezeka kwa 4.3% kutoka tani 769,966.7 mwaka 2021/2022 hadi tani 803,264.3 mwaka 2022/2023 huku uzalishaji wa maziwa ukiongezeka pia kutoka lita bilioni 3.4 mwaka 2021/2022 hadi kufikia lita bilioni 3.6 mwaka 2022/2023 sawa na ongezeko la 5%.
Ulega amesema “Vipande vya ngozi milioni 14.1 vimezalishwa mwaka 2022/2023 ikilinganishwa na vipande milioni 13.6 vilivyozalishwa mwaka 2021/2022, uzalishaji wa mayai umeongezeka kutoka mayai bilioni 4.9 mwaka 2021/2022 hadi bilioni 5.5 mwaka 2022/2023 sawa na ongezeko la 12.2%”
“35% ya kaya zilizopo nchini zinajishughulisha na ufugaji, kati ya hizo 39.3% wanafuga ng’ombe, 36.2 % wanafuga mbuzi, 13.5% wanafuga kondoo na 10.9% wanafuga nguruwe, aidha 55.4% ya kaya hizo pia hujishughulisha na ufugaji wa kuku”