Wizara ya afya huko Gaza inayoendeshwa na Hamas ilisema Jumatatu kuwa watu wasiopungua 32,333 wameuawa katika eneo hilo wakati wa zaidi ya miezi mitano ya vita kati ya Israel na wanamgambo wa Kipalestina.
Idadi hiyo inajumuisha takriban vifo 107 katika muda wa saa 24 zilizopita, taarifa ya wizara hiyo ilisema, na kuongeza kuwa watu 74,694 wamejeruhiwa katika Ukanda wa Gaza tangu vita vilipoanza wakati wapiganaji wa Hamas walipoishambulia Israel tarehe 7 Oktoba.
Wakati huo huo China ilisema Jumatatu kwamba inaunga mkono rasimu ya azimio jipya katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu usitishaji vita wa “mara moja” huko Gaza baada ya Beijing na Moscow siku ya Ijumaa kupinga maandishi ya awali yaliyopendekezwa na Marekani.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Lin Jian amesema, China inaunga mkono rasimu hii ya azimio na kuipongeza Algeria na nchi nyingine za Kiarabu kwa juhudi zao katika suala hili na kuongeza: “Tunatumai Baraza la Usalama litaipitisha haraka iwezekanavyo na kutuma ishara kali kwa kukomesha uhasama”.