Idadi ya vifo kutokana na ajali ya moto iliyotokea katika jengo moja lililoko kwenye kitovu cha biashara mjini Johannesburg, Afrika Kusini, imeongezeka na kufikia 74.
Mkuu wa mji wa Johannesburg Floyd Blink amesema jumla ya watu 74 wamepoteza maisha wakati nyumba waliyokuwa wakiishi iliposhika moto na kuzisababisha familia zaidi ya 200 kupoteza makazi.
Amesema wakazi wa jengo hilo lenye ghorofa tano walikuwa wameunganisha maji na umeme kwa njia haramu.
Bw. Blink amesema hadi kufikia jana, watu 61 walikuwa wanatibiwa katika vituo mbalimbali vya afya ndani na nje ya mji, 16 wamepona na wengine 17 bado wamelazwa, huku wengine wakiendelea kupata huduma katika vitengo vya majeruhi. Pia ameongeza kuwa watawahamisha familia zilizopoteza nyumba katika baadhi ya makazi mjini Johannesburg.