Idadi ya vifo vinavyotokana na Kimbunga Chido nchini Msumbiji imeongezeka hadi 73, maafisa wa usimamizi wa majanga wametangaza Alhamisi.
Katika taarifa mpya, Luisa Meque, Mwenyekiti wa Taasisi ya Kitaifa ya Kudhibiti Hatari za Majanga nchini (INGD), amesema wakati tathmini ikiendelea ya kiwango cha uharibifu uliosababishwa na kimbunga hicho katika taifa hilo la Kusini mwa Afrika, miili zaidi inaendelea kutambuliwa.
“Hatuwezi kufahamu idadi kamili ya watu waliokufa kutokana na dhoruba,” alisema. Meque alisema kuwa idadi ya waliojeruhiwa pia inaongezeka kila siku.
“Hali yetu ni ya kutisha. Tunahitaji msaada mkubwa ili kujua idadi kamili ya walioaga dunia, vyenginevyo, inakuwa vigumu sana kwetu kupata miili, kwa sababu baadhi yao wamezikwa baada ya kuangukiwa na majengo,” alisema.
“Kadiri dhoruba ilivyotulia, kuna uwezekano kwamba idadi ya vifo itaongezeka kwani bado tunatathmini kiwango cha uharibifu,” Meque alisema.