Jarida moja la nchini Marekani limeripoti kuwa takwimu za idadi ya vita vinavyopiganwa katika sehemu mbalimbali duniani zinaonyesha kuwa kumekuwepo na ongezeko tokea mwaka 2010.
Kwa mujibu wa IRNA, jarida la Foreign Affairs la Marekani limeandika katika toleo lake ya siku ya Jumatatu kuwa: idadi, ukubwa na kuchukua muda mrefu mizozo na mapigano duniani kote kuko katika kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu baada ya kumalizika Vita Baridi.
Foreign Affairs limeandika kuwa uchambuzi wa mizozo na mapigano uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Oslo unaonyesha kuwa kulikuwapo na migogoro inayoendelea 55 mnamo mwaka 2022, ikiwa na wastani wa miaka minane hadi 11.
Kulingana na ripoti hiyo, idadi ya vita kote ulimwenguni ilipungua kati ya 1990 na 2007, lakini mnamo 2010, idadi hiyo ilianza kuongezeka.
Jarida la Foreign Affairs limeongeza kuwa vita ambavyo vimesimamishwa vina uwezekano mkubwa wa kupamba moto tena ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, wakati hali hii hutokea kwa wastani wa mara tano kwa mwaka.
Umoja wa Mataifa ulitangaza Januari mwaka huu kwamba idadi ya vita vya mapigano makali duniani imefikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu vilipomalizika Vita vya Pili vya Dunia…/