Hadi watu 3,000 wamekufa na 10,000 hawajulikani walipo katika mafuriko makubwa ambayo yamefunika maeneo ya mashariki mwa Libya.
Msemaji wa Hilali Nyekundu ya Libya Taqfiq Shukri alisema Jumanne kwamba kuna watu 2,084 waliothibitishwa kufariki, huku mkuu wa IFRC Tamer Ramadan akisema: “Idadi ya watu waliopotea inafikia 10,000 kufikia sasa”.
Takriban watu 20,000 wamekimbia makazi yao, kulingana na makadirio. Utawala wa mashariki wa Libya, ulioko Benghazi, unakadiria kuwa watu 3,000 wamekufa.
Katika mji mkuu wa Tripoli, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Abdul Hamid Dbeibah alitangaza Jumanne kwamba ndege ya msaada iliyobeba tani 14 za vifaa na wafanyikazi wa matibabu inaelekea Benghazi kusaidia, ingawa bado kuna ugumu wa kuingia katika jiji lililoathiriwa zaidi la Derna.
Misafara ya misaada inatoka magharibi hadi mashariki katika Libya iliyogawanyika huku serikali ya Tripoli inayotambulika kimataifa ikilitangaza eneo la mashariki kuwa eneo la maafa na kutangaza kutuma msaada.
Utawala wa Benghazi unasema zaidi ya maiti 1,000 zimepatikana katika mji wa Derna ulio katika bahari ya Mediterania.