Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Februari 2, mwaka huu laini za simu milioni 31.4 kati ya laini za simu milioni 43.9 (sawa na asilimia 71.6) zilikuwa zimeshasajiliwa kwa alama za vidole.
Ametoa kauli hiyo leo katika hotuba yake aliyoitoa wakati kuahirisha Mkutano wa 18 wa Bunge jijini Dodoma, ambapo Bunge hilo limeahirishwa hadi Machi 31, mwaka huu.
Amesema zoezi la usajili wa laini za simu ni endelevu na kutumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi ambao hawajasajili laini zao za simu na wale ambao wanaendelea na zoezi la kupata vitambulisho vya uraia na wamekwishapata namba za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), wasajili laini zao za simu kwa mujibu wa sheria.
“Ninatoa wito kwa NIDA, isogeze huduma za kutoa namba za vitambulisho karibu na wananchi kwa kadiri inavyowezekana. Lengo ni kutoa fursa kwa wananchi wengi zaidi ili wapate kupata namba za vitambulisho na kuwawezesha kusajili laini zao za simu na vilevile, kupata Vitambulisho vya Taifa kwa matumizi mengine muhimu,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeendelea na zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa awamu ya kwanza, ambapo hadi kufikia tarehe 2 Februari, 2020, Tume ya Uchaguzi imekamilisha uandikishaji wa wapiga kura katika kanda ndogo 12 kati ya 14 zilizopangwa katika ratiba ya uboreshaji wa awamu ya kwanza.