Idadi ya watu duniani inatarajiwa kufikia bilioni nane katikati mwa Novemba mwaka huu, huku India ikitarajiwa kuipita China mwaka ujao kama nchi yenye watu wengi zaidi, Umoja wa Mataifa umesema katika taarifa.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Jumatatu inatabiri kwamba idadi ya watu duniani inaweza kuongezeka hadi karibu bilioni 8.5 mwaka 2030, hadi bilioni 9.7 mwaka 2050 na kufikia bilioni 10.4 mwaka 2100.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, idadi ya watu duniani inaongezeka kwa kiasi kutokana na kupungua kwa vifo, huku umri wa kuishi duniani ukifikia miaka 72.8 mwaka 2019, ambayo ni takriban miaka tisa zaidi ya ilivyokuwa mwaka 1990. Wakati huo huo, shirika hilo limesema kuwa kasi ya ukuaji inapungua polepole.