Watu wengine 33 wamepimwa na kugunduliwa kuwa na virusi vya mpox nchini Uganda, na kufanya idadi ya waliothibitishwa nchini humo kufikia 69.
Akiongea kwa njia ya simu na Shirika la Habari la China, Xinhua, mkurugenzi wa afya ya umma katika Wizara ya Afya ya Uganda Daniel Kyabayinze, alisema wagonjwa hao wapya waliripotiwa katika wilaya 11 zilizoathiriwa ambapo wengi wao walipata ugonjwa huo kwa sababu ya ngono.
Kyabayinze alisema wilaya ya kati ya Nakasongola, iliandikisha wagonjwa 21 wa mpox, na kuwa kitovu cha virusi hivyo kutokana na shughuli katika baa na nyumba za kulala wageni zinazotembelewa mara kwa mara na wavuvi.
Wizara ya Afya ya Uganda, kwa msaada wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na washirika wengine, imeimarisha hatua za kukinga, ikiwemo kuimarisha ufuatiliaji, kusimamia wagonjwa, mawasiliano hatari na ushiriki wa jamii, na kampeni za uhamasishaji wa umma ili kuzuia kuenea kwa virusi.