Omar Touray Mwenyekiti wa Kamisheni ya Jumuiya ya Ecowas amesema katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa watu laki tano katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (Ecowas) yenye nchi wanachama 15 ni wakimbizi.
Ameongeza kuwa watu wengine karibu milioni 6 na laki mbili wamekuwa wakimbizi wa ndani katika nchi hizo za magharibi mwa Afrika.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Jumuiya ya Ecowas amesema kuwa idadi ya watu wanaohitaji msaada itaongezeka na kufika milioni 42 hadi kufikia mwishoni mwa mwezi ujao wa Agosti iwapo hakutapatikana misaada ya kutosha kutoka nje kwa ajili ya kuwapatia chakula watu milioni 30 wanaohitaji msaada wa haraka.
Omar Touray ametaja masuala kama ugaidi, uasi wa silaha, jinai zilizoratibiwa, kuingia madarakani serikali kinyume na katiba, shughuli haramu za baharini, migogoro ya mazingira na taarifa za uwongo kuwa miongoni mwa mambo yanayosababisha ukosefu wa usalama na kuvuruga uthabiti huko magharibi mwa Afrika.
Amesema, eneo la magharibi mwa Afrika lina wasiwasi kuhusu jeshi kushika hatamu za uongozi; ambapo nchi tatu katika ukanda huo yaani Mali, Burkina Faso na Guinea hivi sasa zinaongozwa na utawala wa kijeshi.