Jumla ya Wanafunzi 3396 kati ya Wanafunzi 4873 sawa na asilimia 69. 58 wameripoti kuanza masomo ya kidato Cha kwanza katika Wilaya ya Muheza huku Wanafunzi 1487 wakiwa hawajaripoti kuanza masomo hayo .
Akizungumza katika ziara yake ya kata Kwa kata yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kukagua miradi ya maendeleo , Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga Halima Bulembo amewataka Wazazi na walezi ambao watoto wao hawajaripoti wahakikishe wanawapeleka shule vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Pia amesema watawachukulia hatua kali za kisheria Wazazi wote wanaowaficha watoto wenye ulemavu ili wasipate haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Bulembo akiwa kata ya Mhamba amesema kuwa watoto waliochaguliwa kwenda kidato cha kwanza katika kata hiyo ni 53 kati ya hao walioripoti ni 27 na 26 hawajaripoti.
Mkuu huyo wa Wilaya yupo katika ziara ya kata Kwa kata ambapo anatarajia kupita katika kata zote 37 zilizopo Wilayani humo.