Shirika la Maendeleo la Serikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) Jumatatu lilitoa wito kwa pande zote zinazopambana za Sudan kusaini makubaliano ya kusitisha vita.
Baada ya mkutano wa siku moja wa viongozi wa nchi za IGAD uliofanyika Addis Ababa nchini Ethiopia, IGAD ilitoa taarifa ikizisihi pande zinazopambana za Sudan zikubali kusitisha vita moja kwa moja bila masharti. Taarifa hiyo pia ilizitaka pande hizo kuacha vurugu mara moja, na kujenga mfumo wa utekelezaji wenye ufanisi na usimamizi.
IGAD pia ilisisitiza wito wake kwa viongozi wa Sudan kuwa na mkutano wa ana kwa ana, ikisema mapambano ya kijeshi yanayoendelea nchini humo hayawezi kutatuliwa kwa njia ya kijeshi.
Mamia ya watu wameuawa na maelfu kujeruhiwa katika mapigano hayo huku mashambulio ya anga na urushianaji wa risasi yakienea katika maeneo mengi ya Khartoum, na kusababisha maelfu ya Wasudan kuhamia nchi jirani.