Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro ametekeleza agizo la Rais John Magufuli la kuwaondoa katika vituo vyao vya kazi, Askari Polisi kwa uzembe kwa kutowajibika ipasavyo hali iliyosababisha kuhujumiwa kwa miundombinu ya reli.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), David Misime, amesema tayari viongozi hao walishaondolewa Mlandizi na nafasi zao kupangiwa wengine.
Kwa mujibu wa Misme, katika mabadiliko hayo, IGP Sirro aliwahamisha aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mlandizi (OCD), Mrakibu wa Polisi (SP) Severine Samwel Msonda na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Mlandizi (OCS), Mrakabu Msaidizi wa Polisi (ASP) Michael Erick Kaniki, kwenda katika Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani.
Amesema Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Gairo, SP Julieth Lyimo, sasa anakuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mlandizi huku Joel Aidanus Mkuche aliyekuwa Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, akitumwa kuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Mlandizi.