Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, amesema kuwa mara baada ya kusikia aliyekuwa mgombea urais wa CHADEMA Tundu Lissu, kwamba anatishiwa na hatimaye kukimbilia ubalozini, alikiandikia barua chama chake kwamba afike polisi kwa ajili ya kueleza undani wa nani anayemtishia.
IGP Sirro ametoa kauli hiyo hii leo DSM, wakati akitoa taarifa ya mwenendo wa usalama wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu na kwamba endapo mtu yeyote akitoa taarifa ya kutishiwa na akaomba ulinzi, yeye yuko tayari kumpa ulinzi wa familia yake.
“Hata alipokuja hapa nchini tumejitahidi sana kumpata tuweze kujua kitu gani kimefanyika lakini hakutaka, tumejitahidi sana mpaka kupeleka barua kwenye chama chake tunamuomba aje hata asindikizwe na Balozi” IGP Sirro
“Hivi ukitishiwa kwa maneno hata silaha jibu lake ni kukimbilia ubalozi, hata mimi nimeshatishiwa kwamba Kamanda Sirro leo tutakushughulikia sasa nakimbia kwenda ubalozi gani, inategemea na mipango mikakati yake” IGP Sirro