Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limetangaza kuwa uchumi wa Burundi unatarajiwa kukua kwa asilimia 4.3 mwaka wa 2024, ongezeko kubwa kutoka ukuaji wa 2.7% mwaka wa 2023.
Mtazamo huu ulioboreshwa unachangiwa na utendaji bora katika sekta ya kilimo, ambayo ina jukumu muhimu katika uchumi wa nchi, hasa kupitia mapato kutoka kwenye zao la chai na kahawa.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, IMF ilibainisha kuwa makadirio ya ukuaji huo yanaungwa mkono na uzalishaji thabiti wa kilimo, uwekezaji wenye tija na mageuzi yanayoendelea kufanyika.
Uhaba wa mafuta ulitatiza shughuli za kiuchumi nchini Burundi mnamo 2023, na nchi inapata ahueni baada ya miaka mingi ya mizozo na ukosefu wa utulivu wa kisiasa.
IMF imeonyesha kuwa mwishoni mwa mwaka jana, akiba ya fedha za kigeni ya Burundi ilifikia dola milioni 96.4.