Waziri wa Nishati January Makamba, amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwenye Mkutano wa Viongozi wa Dunia unaojadili Program ya Afrika ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Africa Adaptation Summit) unaofanyika Rotterdam, Uholanzi leo tarehe 5/9/2022.
*WAZIRI MAKAMBA AMWAKILISHA RAIS SAMIA KWENYE MKUTANO WA VIONGOZI WA DUNIA WA MABADILIKO YA TABIANCHI KWA AFRIKA *
Mkutano huo unalenga kushawishi Washirika wa Maendeleo, Taasisi za Kifedha na Sekta binafsi na marafiki wa Afrika kuchangia fedha kwenye Programu hiyo ya Afrika ambayo inahitaji Dola za Marekani Bilioni 25 ifikapo 2025. Benki ya Maendeleo ya Afrika imechangia Dola za Marekani bilioni 12.5.
Mkutano huu unafanyika kama sehemu ya maandalizi ya mkutano wa 27 nchi wananchama wa mkataba wa mabadiliko ya Tabianchi ambao unatarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu huko Sharm El Sheik Mistri ambako suala la kuhimili mabadiko ya Tabianchi kwa Afrika ni moja ya agenda muhimu ya mkutano huo.
Katika Mkutano Waziri wa Nishati amekutana na Viongozi wa Dunia, Wakuu wa Taasisi na Mashirika mbalimbali na kujadiliana nao fursa mbalimbali ikiwa pamoja na namna bora ya Tanzania kunufaika na Mpango huo wa AFRICA ADAPTATION ACCELERATION PROGRAM (AAAP) ambao utaharakisha mipango ya nchi katika kukabiliana na majanga yakiwemo UVIKO19, ukame, njaa, ajira kwa vijana na mafuriko.
Mkutano huo uliongozwa na Rais wa Jamhuri ya Senegal na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika pamoja Mhe. Macky Sally, na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa pia Mwenyekiti wa Kituo cha kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (GCA) Mhe. Ban Ki-Moon.