Iran siku ya Jumanne ilikataa miito ya nchi za Magharibi ya kuacha vitisho vyake vya kulipiza kisasi dhidi ya Israel kwa mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh mjini Tehran mwishoni mwa mwezi uliopita.
Jamhuri ya Kiislamu na washirika wake wameilaumu Israel kwa mauaji ya Haniyeh mnamo Julai 31 wakati wa ziara yake katika mji mkuu wa Iran kwa ajili ya kuapishwa kwa Rais Masoud Pezeshkian. Israel haijatoa maoni.
Iran imeapa kulipiza kisasi kifo hicho, ambacho kimekuja saa chache baada ya shambulizi la Israel mjini Beirut kumuua kamanda mkuu wa Hezbollah, kundi lenye nguvu la wanamgambo linaloungwa mkono na Iran nchini Lebanon.
Wanadiplomasia wa nchi za Magharibi wamejitahidi kuepusha mzozo mkubwa katika Mashariki ya Kati, ambapo mvutano ulikuwa tayari kutokana na vita vya Israel na Hamas huko Gaza.
Katika taarifa siku ya Jumatatu, Marekani na washirika wake wa Ulaya waliitaka Iran ipunguze kasi.
“Tuliitaka Iran kuzima vitisho vyake vinavyoendelea vya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Israel na kujadili madhara makubwa kwa usalama wa eneo iwapo shambulio kama hilo litatokea,” ilisema taarifa ya pamoja ya Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Marekani.