Iran imewahukumu watu wanane, akiwemo mwanamke, kifungo cha kati ya miaka mitatu hadi 15 kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji ya mwanajeshi, shirika rasmi la habari la nchi hiyo IRNA liliripoti Jumatano.
Tukio hilo lilitokea wakati wa maandamano ya Novemba katika mji wa Karaj, kaskazini mwa Iran.
Hamid Ghare-Hassanlou alipokea kifungo cha miaka 15 jela na wengine watatu, waliotambuliwa kama Reza Aria, Hossein Mohammadi na Mehdi Mohammadi, walihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela, kulingana na IRNA.
Mohammad Amin Akhlaghi, Amin Mehdi Shokrollahi na Farzaneh Ghare-Hassanlou walihukumiwa kifungo cha miaka mitano. Ali Moazzami Goudarzi alipewa miaka mitatu.
Shirika la habari la mahakama la Mizan lilisema hukumu hizo zilitolewa mapema na mahakama ya Karaj na tarehe za maamuzi hayo bado hazijulikani.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu afisa wa ngazi ya juu wa mahakama katika mkoa wa kaskazini wa al-Borz, Hossein Fazeli Harikandi akisema kuwa washitakiwa wanane walihusika katika mauaji ya Ruhollah Ajamian Novemba 2022, mwanachama wa kikosi cha Basij, kinachofanya kazi chini ya Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Waendesha mashtaka walikuwa wamedai kuwa Ajamian alivuliwa nguo na kuuawa na kundi la waombolezaji waliokuwa wakitoa heshima kwa waandamanaji waliouawa wakati wa kukandamiza maandamano ya kupinga serikali.
Kunyongwa kwao kulizua shutuma nyingi huku mashirika ya kutetea haki za binadamu na mawakili wakidai watu hao wawili walipigwa wakiwa kizuizini, kuteswa na kulazimishwa kukiri makosa yao.