Iran imewaita wanadiplomasia wa Uswidi na Denmark katika mji mkuu Tehran kubainisha malalmiko yake makali kuhusu vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu katika nchi hizo mbili za Nordic.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Haki za Kibinadamu ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aliwaita maafisa hao wawili nyakati tofauti siku ya Jumapili.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amelaani vikali kuendelea vitendo viovu na vya kikatili vya kukitusi kitabu kitakatifu cha Waislamu katika nchi hizo mbili na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inaamini kuwa serikali za Uswidi na Denmark zinapaswa kubeba dhima kamili na matokeo mabaya ya vitendo hivyo viovu.
Afisa huyo ametahadharisha zaidi juu ya kuendelea vitendo hivyo ambavyo amevitaja kuwa njama hatari huku akiashiria kauli ya hapo awali iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba kuwaunga mkono wahalifu na wanaoitukana Qur’ani Tukufu ni aina ya kutangaza vita dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu.
Afisa huyo amemaliza mazungumzo yake kwa kusema kuwa licha ya msimamo wa wazi na azma kubwa ya wanazuoni wapenda uhuru duniani katika kulaani kitendo hicho cha kufuru, lakini nchi za Uswidi na Denmark zimeendelea kutojali kufuata maazimio yaliyoidhinishwa na Baraza la Haki za Binadamu na vilevile Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuhusu suala hili.