Israel imeua zaidi ya watoto 13,000 huko Gaza tangu Oktoba 7 huku wengine wakikabiliwa na utapiamlo mkali na hawana “hata nguvu za kulia”, linasema Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF).
“Maelfu zaidi wamejeruhiwa au hatuwezi hata kubaini walipo. Huenda wamekwama kwenye vifusi … Hatujaona kiwango hicho cha vifo miongoni mwa watoto katika takriban vita vingine vyote duniani,” Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell aliambia mtandao wa CBS News siku ya Jumapili.
“Nimekuwa katika wodi za watoto wanaokabiliwa na utapiamlo mkali wa upungufu wa damu, wodi nzima iko kimya kabisa. Kwa sababu watoto, watoto wachanga … hawana hata nguvu ya kulia.”
Russell alisema kulikuwa na “changamoto kubwa sana za ukiritimba” za kuhamisha malori kwenda Gaza kwa msaada na usaidizi huku njaa ikiwakumba zaidi ya Wapalestina milioni mbili tangu vita vya “mauaji ya halaiki” ya Israeli kuanza.