Msichana mwenye umri wa miaka mitatu anayetarajiwa kuwa miongoni mwa mateka walioachiliwa, asema afisa wa Marekani
Wamarekani watatu, akiwemo msichana wa miaka mitatu, wanatarajiwa kuwa miongoni mwa mateka 50 walioachiliwa na Hamas, afisa mkuu wa Marekani amesema.
Afisa huyo hakuwataja raia wa Marekani, lakini alisema wazazi wa msichana mdogo walikuwa miongoni mwa waliouawa wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7 nchini Israel.
Mbali na raia wa Israel, zaidi ya nusu ya mateka wana uraia wa kigeni na wa nchi mbili kutoka baadhi ya nchi 40 zikiwemo Uingereza, Marekani, Ufaransa, Argentina, Ujerumani, Chile, Uhispania na Ureno, serikali ya Israel imesema.
Ufaransa inatumai raia wake wanane wanaoaminika kuwa mateka pia wataachiliwa, waziri wake wa mashauri ya kigeni alisema.
“Tunatumai kuwa kutakuwa na Wafaransa kati ya kundi la kwanza la mateka kuachiliwa,” Catherine Colonna aliiambia redio ya Ufaransa Inter.
Kamisheni ya Masuala ya Wafungwa katika Mamlaka ya Palestina yenye makao yake makuu mjini Ramallah imesema zaidi ya Wapalestina 7,800 wamefungwa na Israel wakiwemo wanawake 85 na watoto 350.
Wengi wao walizuiliwa bila kufunguliwa mashtaka au kwa matukio kama vile kuwarushia mawe wanajeshi wa Israel, na si kwa kuanzisha mashambulizi ya wanamgambo, iliongeza.
Israel inatazamiwa kuwaachia huru wafungwa 150 wa Kipalestina ili kuwalipa mateka 50 wanaoachiliwa.