Benjamin Netanyahu amesema Israel inaweza “kujitegemea” baada ya Marekani kuonya kuwa inaweza kusitisha usambazaji wa silaha ikiwa waziri mkuu wa Israel ataamuru uvamizi kamili wa Rafah huko Gaza.
“Tukihitaji tutajitegemea. Nimesema ikibidi tutapigana kwa jino na ukucha,” alisema.
Rais wa Marekani Joe Biden alisema atazuia baadhi ya silaha ikiwa ni pamoja na mizinga ikiwa Rafah itavamiwa.
Marekani tayari imesitisha shehena ya mabomu kutokana na hofu ya vifo vya raia.
Bw Netanyahu siku ya Alhamisi hata hivyo alikariri vita vya mwaka 1948 vya kutupilia mbali maonyo kutoka Marekani, mshirika wa karibu wa Israel.
“Katika Vita vya Uhuru miaka 76 iliyopita, tulikuwa wachache dhidi ya wengi,” alisema “Hatukuwa na silaha. Kulikuwa na vikwazo vya silaha kwa Israel, lakini kwa nguvu kubwa ya kiroho, ushujaa na umoja kati yetu – sisi tulikuwa washindi.”
Alisema kuwa Israel ina “zaidi ya kucha zetu” ikiwa Bw Biden atasitisha usambazaji wa silaha. “Na kwa nguvu hiyo ya kiroho, kwa msaada wa Mungu, pamoja tutakuwa washindi.”
Yoav Gallant, waziri wa ulinzi wa Bw Netanyahu, wakati huo huo alisema “maadui wa Israel pamoja na … marafiki bora” wanapaswa kuelewa kwamba nchi yake “haiwezi kutawaliwa. Tutasimama imara, tutafikia malengo yetu.”
Maoni hayo yanawadia saa chache baada ya Umoja wa Mataifa kusema zaidi ya watu 80,000 wametoroka Rafah tangu Jumatatu huku kukiwa na mashambulizi ya mara kwa mara na vifaru vya Israel vikikusanyika karibu na maeneo yaliyojengwa.