Israel imejipanga kuwafurusha mamia ya Waarabu na wakaazi kutoka Jerusalem Mashariki hadi maeneo ya Mamlaka ya Palestina, ikitaja madai ya kuwa na uhusiano na ugaidi, kwa mujibu wa redio ya jeshi la Israel.
“Israel iko mbioni kuwafukuza mamia ya Waarabu wa Israel na wakaazi wa Jerusalem Mashariki ambao wamepatikana na hatia ya ugaidi katika maeneo ya Mamlaka ya Palestina, huku baadhi yao wakitarajiwa kufukuzwa katika miezi ijayo,” ilisema.
Hatua hii inajiri baada ya marekebisho ya Sheria ya Uraia iliyotolewa Februari mwaka jana, kulingana na kituo cha redio.
“Israel iko mbioni kuwatimua magaidi 18 katika maeneo ya Mamlaka ya Palestina katika awamu ya kwanza, huku mamia ya wanaharakati wengine wakilengwa kuwanyang’anya uraia wao au kufuta ukaazi wao,” ilisema.
Wakati raia wa Kiarabu wana uraia wa Israel, Wapalestina katika Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu wana hadhi ya ukaaji wa kudumu.
Kituo hicho cha redio kilibainisha kuwa “Mamlaka ya Vita vya Kiuchumi dhidi ya Ugaidi, kwa ushirikiano na jeshi la Israel na wakala wa usalama wa Shin Bet, imehitimisha ripoti ya kijasusi kuhusu fedha zilizohamishwa na Mamlaka ya Palestina kwa magaidi (wafungwa wa Kipalestina walioachiliwa) wanaoshikilia uraia au ukaazi wa Israel. .”