Israel na Hamas haziko karibu na makubaliano ya kusitisha uhasama huko Gaza na kuwaachilia mateka, mpatanishi wa Qatar alisema siku ya Jumanne, akionya kuwa hali bado ni “ngumu sana”.
Licha ya wiki kadhaa za mazungumzo yaliyohusisha wapatanishi wa Marekani, Qatar na Misri, mwezi mtukufu wa Waislamu wa Ramadhani ulianza Jumatatu bila ya kuanza kwa mapatano na kubadilishana mateka.
“Hatuko karibu na makubaliano, kumaanisha kwamba hatuoni pande zote mbili zikikutana kwa lugha ambayo inaweza kutatua kutokubaliana kwa sasa juu ya utekelezaji wa makubaliano,” msemaji wa wizara ya mambo ya nje Majed al-Ansari aliambia mkutano wa waandishi wa habari.
Pande zote zilikuwa “zinaendelea kufanya kazi katika mazungumzo ili kufikia makubaliano kwa matumaini ndani ya mipaka ya Ramadhani,” Ansari alisema.
Lakini aliongeza kuwa hawezi “kutoa ratiba yoyote” juu ya mpango huo na akaeleza kuwa mzozo ulibaki “mgumu sana”.