Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Ubelgiji ametoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu jinai za kivita zinazofanywa na utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Akizungumza katika mahojiano ya televisheni jana jioni, Caroline Gennez, Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Ubelgiji amegusia jinai na uhalifu unaoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Gaza na kusema: “Israel inapasa kuchunguzwa kwa kufanya jinai za kivita, na ushahidi uliopo unanyesha kuwa utawala huo umetenda uhalifu wa kivita.”
Gennez ameongeza kuwa: “Katika kukabiliana na mashambulizi ya Hamas, Israel inawaadhibu raia wasio na hatia na kukiuka sheria za vita.”
Waziri huyo wa serikali ya Ubelgiji ameitaka serikali ya nchi hiyo kuchunguza hatua za kukabiliana na na uhalifu unaofanywa na Israel, ikiwa ni pamoja na vikwazo vya uagizaji wa bidhaa za utawala wa Kizayuni na kuzuia utoaji wa viza kwa maafisa wakuu wa utawala huo.
Uhalifu na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala katili wa Israel dhidi ya watu wa Gaza yamechochea hasira za watu kote duniani.