Takriban wanajeshi 258 wa Israel wameuawa tangu shambulio la umwagaji damu lililoanzishwa tarehe 7 Oktoba na kundi la wanamgambo wa Hamas kutoka Palestina dhidi ya Israel, jeshi la Israel limesema Ijumaa, Oktoba 13.
“Familia za wanajeshi 258 ambazo zimewapoteza wapendwa wao zimefahamishwa rasmi,” msemaji wa jeshi Daniel Hagari amesema katika mkutano na wanahabari. Ripoti ya awali inaonyesha askari 169 waliuawa, shirika la habari la AFP linabaini.
Wakati huo huo ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu imetoa ombi la dharura ikizitaka nchi kutoa $294m (£241m) kwa ajili ya ufadhili wa dharura wa mahitaji ya haraka zaidi ya Wapalestina.
Fedha hizo zitatumika kuwasaidia baadhi ya watu milioni 1.2, shirika hilo lilisema.
Zaidi ya watu 84,000 katika mji wa Gaza walikosa makazi siku ya Alhamisi, shirika hilo lilisema, na kuongeza kuwa sasa kuna zaidi ya watu 423,000 wasio na makazi huko.