Kampuni inayoongoza katika uendeshaji wa michezo ya bahati nasibu za taifa barani Afrika, ITHUBA Africa kwa kushirikiana na kampuni ya Kitanzania, SF Group wametangaza rasmi kuingia katika soko la Tanzania.
Hatua hiyo imekuja baada ya kukabidhiwa rasmi leseni ya uendeshaji wa mchezo wa Bahati Nasibu ya Taifa kwenye hafla fupi iliyofanyika tarehe 28 Juni katika ofisi za Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania jiijni Dar es Salaam.
Makabidhiano hayo ni hatua muhimu katika kufikia dhamira ya ITHUBA ya kuchagiza maendeleo ya kijamii na kiuchumi barani Afrika. Kupitia uwekezaji wa dola za kimarekani milioni 20, ITHUBA na SF Group wamedhamiria kuleta mapinduzi katika soko la michezo ya bahati nasibu kupitia ubunifu katika usanifu wa jukwaa la michezo hiyo.
Makabidhiano hayo ya leseni yalitanguliwa na hafla ya utiaji saini iliyofanyika Mei 8, 2024 na kuhudhuriwa na wafanyakazi wa ITHUBA na SF Group wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa SF Group – mfanyabiashara mahiri – Kelvin Koka.
Wengine waliohudhuria hafla ya utiaji saini ni pamoja na wajumbe wa Bodi, Mkurugenzi Mkuu, pamoja na Menejimenti ya Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Balozi Modest J. Mero.
Akizungumzia matukio hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa ITHUBA, Charmaine Mabuza alisema, “Tunayo furaha kubwa kuungana na SF Group na kutuwezesha kuunganisha teknolojia na ujuzi wetu pamoja na uzoefu wao wa soko la Tanzania. Wapenzi wa mchezo wa bahati nasibu hapa Tanzania wataweza kushiriki katika michezo ya kipekee kupitia jukwaa lililoundwa maalumu kwa ajili ya soko la Tanzania. Washiriki watapata fursa ya kucheza michezo mipya ya kusisimua na kupata ofa mbalimbali ambazo pia zitachangia katika kuleta mabadiliko kwenye uchumi wa jamii.”
ITHUBA na SF Group wanajipanga kuwakaribisha wafanyabiashara kujisajili kama wauzaji wa bidhaa za ITHUBA hapa nchini. Wafanyabiashara watanufaika na malipo ya kamisheni na pia kuvutia wateja zaidi katika maduka yao kutokana na mauzo ya tiketi za bahati nasibu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Michezo ya Bahati Nasibu nchini Tanzania, Balozi Mero ameikaribisha ITHUBA pamoja na SF Group kusukuma gurudumu la michezo hiyo nchini; “Tunayo furaha kuikaribisha ITHUBA iliyoingia ubia na kampuni ya Kitanzania, SF Group kuendesha michezo ya bahati nasibu ya taifa. Ubia wao ni fursa nzuri ya kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini kupitia mapato yatakayotokana na michezo ya bahati nasibu ya taifa. Tuna shauku kubwa kufanya kazi kwa ukaribu na ITHUBA ili kuleta mabadiliko chanya na kuboresha maisha ya Watanzania.”
Kwa ujio wa ITHUBA nchini Tanzania, mchezo wa Bahati Nasibu ya Taifa utakuwa kichocheo katika kubadilisha maisha na kuleta mabadiliko chanya miongoni mwa Watanzania.