Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma jana tarehe 28 Mei, 2024 aliungana na Majaji Wakuu kutoka nchi mbalimbali Duniani katika maadhimisho ya miaka 100 ya kuanzishwa kwa Mahakama huru nchini Ireland.
Maadhimisho hayo yalifanyika katika Jengo la Mahakama ya Upeo (Supreme Court) lililopo Mji Mkuu wa Dublin na yalihudhuriwa na Majaji Wakuu pamoja na Marais wa Mahakama za Upeo kutoka Nchi za Wanachama wa Jumuiya ya Ulaya (European Union), Rais pamoja na Majaji wa Mahakama ya Haki za Binadamu ya Jumuiya ya Ulaya. Vilevile kulikuwa na Washiriki kutoka Jumuiya ya Madola akiwemo Jaji kutoka Mahakama ya Upeo ya Uingereza, Jaji kutoka Mahakama ya Upeo ya India.
Katika muendelezo wa sherehe hizo washiriki wote walikaribishwa katika hafla maalum iliyoandaliwa na Rais wa Jamhuri ya Ireland, Mhe. Michael Higgins ambaye wakati akisalimiana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Juma alizungumzia namna ambavyo alitembelea Tanzania miaka ya 1960.
“Wakati nikiwa kijana na mwanzoni mwa maisha yangu ya kisiasa nilitembelea Tanzania, niliguswa sana na maisha pamoja na Uongozi wa Rais wa Kwanza wa Tanzania na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,” alisema Mhe. Higgins huku akiongeza kuwa, Tanzania na Ireland zina historia kubwa kwa miaka mingi.
Maadhimisho hayo yalitanguliwa na wageni kuzungushwa katika maeneo mbalimbali ya Mahakama hiyo pamoja na kupewa historia ya Mahakama hiyo ambapo wageni walipata maelezo ya kina kuhusiana na uanzishwaji wa Mahakama Huru nchini Ireland na baadaye kufuatiwa na sherehe iliyofanyika katika Mahakama ya Upeo.
Baada ya hapo washiriki walikaribishwa kwenye chakula cha usiku na Jaji Mkuu wa Ireland, Mhe. Donal O’Donnell katika ukumbi wa Chama cha Mawakili (Honorable Society of King’s Inns).
Maadhimisho hayo yalifanyika kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Mahakama Huru za nchini Ireland mwaka 1924.
Mahakama Huru za Ireland zilianzishwa mwaka 1924 kufutia uhuru wa Ireland kutoka Ukoloni wa Muingereza na kabla ya hapo Mahakama zote za Ireland kama ilivyokuwa kwa Makoloni mengine ya Muingereza zilikuwa chini ya Sheria ya Uingereza na Maafisa wa Kiingereza.
Jaji Mkuu wa Tanzania yupo Jamhuri ya Ireland baada ya kutembelea Ireland ya Kaskazini kwa mwaliko wa Jaji Mkuu wa Ireland ya Kaskazini na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Ireland ambapo pamoja na mambo mengine leo atapata fursa ya kutoa muhadhara kwenye Taasisi ya Kimataifa na Masuala ya Jumuiya ya Ulaya (Institute of International and European Affairs).
Safari hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa makubalino kati ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Taasisi isiyo ya kiserikali ya nchini Ireland ya (Irish Rule of Law International), makubalino hayo yana lengo la kuwajengea uwezo Maafisa wa Mahakama kutoka Tanzania, Ireland ya Kaskazini na Jamhuri ya Ireland kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania.
Mhe. Prof. Juma ameambatana na Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia na Mirathi-Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa.