Kijana aitwaye Abraham Nduba, mwenye umri wa miaka 26 kutoka kaunti ya Murang’a nchini Kenya amekamatwa na kutupwa jela miaka mitano baada ya kuungama kanisani kwamba ni mwanachama wa genge la uhalifu eneo hilo.
Kijana huyo anayedaiwa kuwa ni jambazi sugu alifika kanisani akiwa mchangamfu na tayari kumpokea Yesu Kristu kama mkombozi wa maisha yake na alikiri kuwa mwanachama wa kundi la Gaica huku akitubu dhambi zake katika kanisa la Kianglikana la Maragua.
Inaripotiwa kwamba Nduba alikwenda kanisani humo bila kufahamu kwamba alikuwa anaandamwa na kikosi kizima cha Polisi.
Nduba aliingia kanisani bila kujua alikuwa ameketi pamoja na maafisa wa polisi waliokuwa wamevalia kiraia. Walimpa muda kutubu dhambi zake zote na kukubali kuishi maisha mapya kama pamba.
Punde baada ya ibada, pasta wa kanisa hilo Peter Kariuki aliarifiwa na polisi amsindikize Ndiba hadi katika Kituo cha Polisi cha Maragua ili ajisalimishe.
Pasta huyo alisimulia namna aliingiza baridi polisi walipomunyoshea bunduki na kuwaomba wamruhusu amwombee kondoo wake ambapo walikubali.
Kwa mujibu wa gazeti la Taifa Leo, Jumanne, Aprili 13, 2021 Abraham Nduba, mwenye miaka 26, alikamatwa mwezi mmoja baada ya kukwepa mtego wa polisi.
Nduba alikiri kuwa mwanachama wa kundi la Gaica huku akitubu dhambi zake katika kanisa la Kiangilakana la Maragua ambapo alikuwa amekwenda kuokoka.
Alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Sivai Agade, siku ya Jumatatu, Aprili 4,2021 ambapo alishtakiwa na makosa matatu ya uhalifu, uuzaji wa pombe haramu na kumiliki kampuni ya kutengeneza pombe haramu.
Nduba aliungama makosa yake na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani au faini ya KSh2 milioni.