Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaadhimisha leo kumbukumbu ya miaka 63 ya uhuru bila mamlaka yake kuwa na udhibiti wa sehemu ya eneo lake lililokaliwa kwa mwaka mmoja na waasi wa M23 wanaosaidiwa na Rwanda, kulingana na shutuma za mamlaka ya DRC, Umoja wa Mataifa na balozi kadhaa za nchi za Magharibi, madai ambayo yanakanushwa na Kigali.
Katika ujumbe wake rasmi jana usiku, Rais Félix Tshisekedi, aliye madarakani tangu mwaka 2019, aliwahakikishia wananchi wake, hata kama katika masuala ya kijeshi na kidiplomasia kuna hali ya kutatanisha.
“Uadilifu wetu wa eneo unatishiwa na jeshi vamizi la kigeni .” Neno la huzuni lilimtoka rais katika hotuba yake ya dakika kumi na tano iliyorushwa muda mfupi kabla ya saa sita usiku kwenye televisheni ya taifa. Felix Tshisekedi kwa mara nyingine tena ameelekeza lawama zake kwa Rwanda, jirani yake anayemtaja kuwa “mwasi kwa jina la maslahi yasiyoeleweka na ya kudharauliwa”.
“Baadhi ya wenzetu kwa wakati huu sahihi katika Mashariki hawawezi kufurahia uhuru huu tunaosherehekea kwa sababu ni waathiriwa wa ukandamizaji wa mvamizi. Ningependa kueleza masikitiko yetu kwao na kuwahakikishia dhamira yetu ya kufanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya kukombolewa kwao kwa uhakika”.
Rais Tshisekedi amekaribisha “ujasiri na nguvu” za vikosi vya ulinzi na usalama vya nchi na kuhimiza serikali yake “kuendelea kudumisha juhudi hii dhidi ya mvamizi yeyote katika ardhi ya mababu zetu, hasa kumuangamiza yeyote anayejaribu kutishia usalama”.
Rais huyo bado ana nia ya dhati ya kufanyika kwa uchaguzi wa urais pamoja na uchaguzi wa wabunge utakaofanyika tarehe 20 Desemba 2023. “Pamoja na kuwepo kwa vikwazo mbalimbali, nawaomba CENI waendelee kwa ujasiri na bila kuzindua upya juhudi zinazoendelea kwa nia ya kuheshimu makataa ya kikatiba katika kuandaa chaguzi mbalimbali kwa mujibu wa viwango vya kimataifa”.
Rais Tshisekedi amesisitiza kuwepo kwa uchaguzi wa “wazi na wa kuaminika”, hata kama yeye mwenyewe anashutumiwa kwa kutosikiza matakwa ya upinzani na kujaribu kupitisha kwa nguvu baadhi ya sheria.