Wananchi wa Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera hususani kata ya Kitendaguro tayari wameanza kunufaika na uwepo wa kituo cha kutolea huduma ya Afya (Pasaka Health care dispensary),na hii inakuja baada ya ndoto ya Kijana Paskalinah iliyodumu kwa muda mrefu ya kumiliki kituo chake cha afya kufanikiwa.
Paskalinah ambaye ni mama wa watoto watatu anasema alipata ndoto hiyo iliyodumu kwa muda mrefu lengo ikiwa ni kusaidia jamii juu ya matatizo mbalimbali ya kiafya na si biashara kwa sasa kwani anaamini kuna watu wengi wanapoteza maisha pengine kwa kukosa gharama za kumudu matibabu yao.
Baada ya kufanikiwa kufungua kituo hicho katika eneo la Kitendaguro,pamoja na kutoa huduma nyingine za matibabu ameanzisha utaratibu wa kutoa huduma bure kwa watoto mapacha chini ya miaka 5 na hii anasema kwake ni kama kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu maana mmoja kati ya watoto wake mapacha alipitia changamoto kubwa ya kiafya mpaka kupelekea kwenda matibabu nchini India na sasa hivi Afya yake iko vizuri.
Kupitia mawazo yake ya kuamua kusaidia jamii hususani upande wa afya iliwagusa watu wengi akiwemo Innocent Mwesiga ambaye ni Mtanzania mzaliwa wa Kitendaguro Manispaa ya Bukoba lakini makazi yake kwa sasa yapo Nchini Marekani,ameamua kumuunga mkono kwa kuongeza huduma nyingine ya kijamii bure (Cocunula diabetric program) ambayo wanapima sukari bure kwa wakazi wa eneo hilo huku akisema kuwa na yeye ameamua kufanya hivo kama kumuenzi mama yake kwa kuwasaidia wananchi wa nyumbani kwao kwani mama yake alifariki kwa ugonjwa wa sukari na anaamini kwa kufanya hivo atakuwa amesaidia kuimarisha afya za watu wengi dhidi ya ugonjwa huo
Aidha baada ya uzinduzi huo uliofanywa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba Godson Gypson, amefurahishwa na uwekezaji huo ambao moja kwa moja umejielekeza kuisaidia jamii,na amewataka wananchi kutumia fursa hiyo hususani kupima sukari ikiwa ni sambamba na kuendelea kuwaunga mkono ili kituo hicho kiweze kudumu kwa muda mrefu.