Wizara ya Maliasili na Utalii inawahamasisha wananchi kujenga makumbusho kwenye maeneo yenye historia ili kuhifadhi na kuendeleza historia lakini pia kujipatia kipato.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) alipokuwa akijibu swali la Mhe. Francis Kumba Ndulane (Mb) aliyetaka kujua Serikali itajenga lini Jengo la Makumbusho katika kijiji cha Nandete ili kuhifadhi Kumbukumbu za Vita ya Majimaji.
Aidha Mhe. Kitandula alisema kuwa ujenzi wa Makumbusho unahitaji utafiti wa kina wa historia ya eneo husika ili kuweza kupata taarifa na mikusanyo itakayowekwa kwenye makumbusho tarajiwa.
‘Kwa kutambua umuhimu wa historia ya vita ya Majimaji katika eneo la Nandete, Serikali kwa kushirikiana na Wadau imeanza kufanya utafiti kwenye eneo hili’ Aliongeza Mhe. Kitandula.
Vilevile Mhe. Kitandula aliongeza kuwa mwaka 2022 Serikali ilifanya maboresho ya Sheria ya Mambo ya Kale Sura 333 ili kuruhusu watu binafsi na Taasisi mbalimbali kuanzisha makumbusho binafsi kwa lengo la kuhifadhi na kuendeleza utalii unaohusiana na utajiri wa kihistoria uliopo eneo husika.