Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekwama kuanza kusikiliza ushahidi wa kesi ya uchochezi inayomkabili, Kiongozi wa ACT Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kwa sababu shahidi amepata dharura.
Kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi lakini Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga amedai shahidi amepata dharura.
Wakili Katuga ameieleza mahakama kuwa walipanga kuwa na shahidi lakini kwa bahati mbaya amepata matatizo ya Kifamilia, hivyo wanaomba ahirisho fupi.
Baada ya kueleza hayo, Wakili wa Zitto, Jebrah Kambole aliiomba mahakama iahirishe kesi hiyo hadi February 27, huku akidai kuwa mtuhumiwa alijipanga kusikiliza kesi hiyo licha ya kuwa anakabiliwa na majukumu mengine.
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi February 27,2019.Zitto alifikishwa Mahakama ya Kisutu kwa mara ya kwanza, Novemba 2, 2018 kujibu mashtaka matatu ya uchochezi katika kesi ya jinai namba 327/2018.
Katika kesi ya msingi, Zitto anadaiwa kutenda makosa hayo, Oktoba 28,2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo.