Kupanuka na kuenea kwa mitandao ya kijamii kuna nafasi muhimu katika maisha ya kila siku ya wanadamu, hasa kwa vijana.
Kupakua na kuweka programu za mitandao ya kijamii kwenye simu, runinga na kadhalika kunahesabiwa kuwa hatua ya kwanza na rahisi zaidi ya kuingia kwenye ulimwengu pepe (virtual world) ambao siku hizi watu wengi wamezama ndani yake.
Ulimwengu pepe, kama zilivyo teknolojia nyingine nyingi zinazotengenezwa na binadamu, una faida na hasara zake mahsusi kwa msingi huo tunatumia fursa hii kuchunguza umuhimu na athari chanya na hasi za mitandao hiyo kwa jamii na maisha yetu.
Miongoni mwa athari chanya za mitandao hiyo kwa maisha ya kila siku ya watu ni kupata taarifa na habari za hivi punde, kujaza wakati wa bure, kuwasiliana kirahisi na familia na marafiki, na kuunda vikundi vya kirafiki, kikazi na kadhalika.
Katika mitandao hiyo ya kijamii watu wanaweza kuwasiliana kwa urahisi na wapendwa wao walioko katika kona zote za duniani na kupata habari zao.
Hii leo, mitandao ya kijamii ni sehemu muhimu ya muundo wa mawasiliano, na wakati huo huo miongoni mwa sababu muhimu zaidi za mabadiliko yanayoshuhudiwa katika mtindo wa maisha, ambayo yameathiri jinsi watu wanavyozungumza, jinsi wanavyojikwatua na kuvaa, nyakati zao za kulala na kupumzika na kadhalika.
Mbali na mtindo wa maisha, mitandao ya kijamii imeweza kuibua maadili mapya au mifumo ya thamani ambayo imeonekana katika mifumo ya kitamaduni ya tabia za watu na hata upatikanaji wa taarifa.
Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vina sifa nyingine muhimu, ikiwa ni pamoja na kwamba vimewafanya watazamaji na wafuatiliaji wengi wa vyombo vya habari kuwa wanaharakati katika tasnia hii ya habari na mawasiliano, utayarishaji na usambazaji wa habari sasa haudhibitiwi tena na vyombo maalumu vya habari, na kila mtumiaji anaweza kuzalisha na kuzambaza habari zake.
Hapana shaka kuwa, sambamba na faida hizi, uwezekano wa kueneza habari zisizo za kweli au zenye madhara kwa watazamaji.
Utafiti uliofanywa na watafiti wa tabia na sayansi ya jamii unaonyesha kuwa, kuna uhusiano mkubwa kati ya matumizi yasiyofaa na ya kupita kiasi ya mitandao ya kijamii na matatizo ya kiakili na kisaikolojia; na mitandao ya kijamii inaweza kusababisha matatizo katika afya ya akili ya watu ambayo wakati mwingine hayawezi kufidiwa.
Katika ulimwengu wa sasa, wengi wetu tunategemea mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter, Snapchat, YouTube, Tik Tok, na Instagram kuwasiliana. Pamoja na hayo ni muhimu kutambua kuwa mitandao ya kijamii na nimuhimu kutambua kuwa haiwezi kamwe kuchukua nafasi ya mawasiliano halisi na ya moja kwa moja baina ya binadamu hivyo ni muhimu kutumia mitandao kwa faida na sivinginevyo.